Saturday, September 1, 2018

Usajili Rock City Marathon waanza rasmi.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dk. Philis Nyimbi (katikati) akisaini fomu za ushiriki wa mbio za Rock City Marathon msimu wa mwaka 2018 wakati hafla fupi ya uzinduzi huo iliyofanyika mkoani humo ambapo alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw John Mongella alieahidi kushiriki mbio hizo. Anaeshuhudia ni Makamu Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mbio hizo Bw Zenno Ngowi (kulia) na Mwakilishi wa Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza (MWAA), Samweli Chakala.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dk. Philis Nyimbi (kushoto) akikabidhi fomu za ushiriki wa mbio za  Rock City Marathon msimu wa mwaka 2018 kwa Mwenyekiti wa mbio hizo Bw Zenno Ngowi wakati hafla fupi ya uzinduzi huo iliyofanyika mkoani humo. Dk Nyimbi pia alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw John Mongella alieahidi kushiriki mbio hizo.NA OSCAR MIHAYO
MWANZA.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mheshimiwa John Mongella leo amekuwa mshiriki wa kwanza kujisajili kushiriki mbio za Rock City Marathon zinazotarajiwa kufanyika October 28 mwaka huu katika viwanja vya CCM Kirumba  jijini humo.

Katika zoezi hilo, RC Mongella alieahidi kushiriki mbio za km 5, aliwawakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dk. Philis Nyimbi.

Akifikisha salamu za RC Mongella, kwenye hafla fupi ya uzinduzi huo iliyofanyika mkoani humo, Dk Nyimbi alisema lengo ni kuonyesha nia ya dhati ya kuunga mkono kauli mbiu ya mbio hizo ambayo ni kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo kanda ya Ziwa ili kuongeza pato la Mkoa pamoja na kuinua mchezo huo uliolipatia taifa heshima miaka ya nyuma.

“Nitoe wito kwa wadau wa michezo na utalii katika kanda yetu ya Ziwa kuhakikisha kwamba  wanayatumia vizuri mashindano haya, kwanza katika kutangaza fursa na vivutio vya utalii vilivyopo kwenye ukanda wetu pamoja  na kukuza vipaji vya mchezo huu’’ alisema.

Mbio hizo tayari zimefanikiwa kuvutia wadhamini kadhaa wakiwemo kampuni za Puma Energy Tanzania, Tiper, Nmb, Tawa, Tanapa, Ttb, Nssf, Sds, Gold Crest, New Mwanza Hotel,  Cf Hospital, CocaCola, Metro Fm, Ef Outdoor, Tonito, Kk Security, Belmont Fairmount Hotel , Bigie Customs na Global Education Link.

Pamoja na kuwapongeza waandaaji wa mbio hizo kampuni ya Capital Plus International, Dk Nyimbi alitoa wito  kwa waandaaji  hao kushirikiana na viongozi wa mchezo huo hapa nchini kuhakikisha wanakuwa na mkakati wa kudumu unaolenga kuwaandaa washiriki kutoka ndani ya nchi ili waweze kuleta matokeo mazuri dhidi ya washiriki kutoka mataifa ya nje.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mbio hizo, Bw Zenno Ngowi aliwasihi washiriki wanaotoka ndani ya nchi kufanya maandalizi ya kutosha kutokana na ushindani mkubwa unaotarajiwa kutoka kwa washiriki wa nje ya nchi ambao, kwa mujibu wake wameonesha mwitikio mkubwa wa kushiriki katika mbio hizo.

“Lengo sio kuwatisha ila sisi kama waandaaji wazalendo tunafarijika zaidi tukiona watanzania wenzetu wanaibuka washindi kwenye mashindano haya. Tofauti na mashindano yaliyopita mwaka huu ushiriki wa majirani zetu kutoka Kenya na Ethiopia  utakuwa mkubwa sana na sisi tunawakaribisha,’’ alisema.

Bw Ngowi alivitaja vituo vitakavyohusishwa katika usajili huo kuwa ni pamoja na Igoma, Buzuruga, Airport Mwanza, Rock city mall, Chuo Kikuu cha Saut, Nyegezi Stand, Mwanza hotel, Nyamagana Stadium, Dampo pamoja na Nyakato.

Alisema usajili huo pia utahusisha ofisi zote za riadha mikoa ya Geita, Simiyu na Shinyanga.

 “Mwaka huu tumeongeza idadi ya vituo vya usajili wa mbio hizi lengo likiwa ni kuwafikia washiriki wengi zaidi ambapo pia kwa upande wa Dar es Salaam usajili utafanyika maeneo ya Mlimani City,” alisema.

Aliongeza kuwa katika kurahisisha zaidi zoezi hilo, usajili wa mwaka huu pia utafanyika kwa njia ya simu kupitia huduma ya M-Pesa.

“Tupo kwenye hatua za mwisho kuhakikisha kwamba washiriki wa mbio hizo wanaweza kujisajili kupitia huduma ya M-PESA ili kuokoa muda na kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa ufanisi zaidi likihusisha eneo kubwa la nchi kwa kuwa huduma ya M-PESA inapatikana kila kona ya nchi,’’ alisema.

Alisema usajili huo utahusisha mbio za km 42 kwa wanaume na wanawake, Kilomita 21 kwa wanaume na wanawake, km 5 kwa washiriki kutoka kwenye mashirika (Corporates) na walemavu wa ngozi, km 3 kwa wazee wenye umri kuanzia miaka 55 na kuendelea pamoja na km 2.5 kwa watoto wenye umri wa miaka 7 hadi 10.


SHARE THIS

Facebook Comment

0 comments: