Wednesday, September 5, 2018

Precision Air kuanza ruti mpya ya kwenda Chato na Dodoma.- Famara Media Group


Shirika la Ndege la Precision limesema linatarajia kuanza safari za kwenda Chato na Dodoma kuanzia mapema mwakani.

Likiwa na miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, shirika hilo linafanya takriban safari 10 za ndani na sasa linajipanga kuanza kuwahudumia wateja wake waliopo kanda ya ziwa pamoja na wale wa makao makuu ya nchi.

Akizungumza leo Septemba 5, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Precision, Hillary Mremi amesema wamegundua kuna fursa ya kutanua soko lao endapo watakuwa na safari za kwenda na kurudi Chato pamoja na Dodoma hivyo wameshaanza kutathimini masoko hayo ili kuandaa safari zitakazokidhi mahitaji.

“Kati ya Machi na Oktoba mwakani tutazindua safari hizo. Kumekuwa na matukio muhimu katika maeneo haya na hatua ya Serekali kuhamia Dodoma ni dhahiri itaongeza safari za watu kwenda na kutoka Dodoma,” amesema Mremi.
Amefafanua kuwa wamedhamiria kuanzisha safari za Dodoma ili kuwawezesha wasafiri kuunganisha safari zao kwenda makao makuu ya nchi.

Kuhusu Chato amesema ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Chato umefungua milango kwa Precision Air kujitanua zaidi kanda wa ziwa na watalenga kuuhudumia zaidi Mkoa wa Geita ambao una shughuli nyingi za uchumi ikiwamo uchimbaji wa madini, uvuvi na utalii.

“Uboreshaji wa viwanja vya ndege kunatuwezesha kuanzisha safari nyingi zaidi ambazo zitaifungua nchi na kuongeza kasi ya maendeleo. Tuaanzisha safari zetu za Chato na Dodoma mwakani,” amesema.

Precision Air linakuwa shirika la kwanza kutangaza kuanza kutua katika Uwanja wa Chato. Kwa sasa shirika hilo linafanya safari kutoka Dar es Salaam kuelekea Arusha, Bukoba, Kahama, Kilimanjaro, Musoma, Mtwara, Mwanza, Tabora, Zanzibar, Seronera, Nairobi na Entebbe.

SHARE THIS

Facebook Comment

0 comments: