Sunday, September 2, 2018

Mashabiki na wadau wa soka Mkoani Mwanza watoa ushauri kuhusu matokeo mabaya inayoyapata timu ya Alliance Fc- Famara Media Group

Mwandishi Wetu @FMG
Mwanza.
Wadau mbalimbali wa soka mkoani Mwanza wametoa mapendekezo kuhusu nini kifanyike ili timu yao ipate matokeo kwenye michuano ya ligi kuu Tanzania bara inayoendelea kushika kasi nchini.

Kauli hizi zimekuja muda mfupi baada ya Afisa Habari wa timu hiyo Jackson Luka Mwafulango kuandika andiko linalotoa ufafanuzi kuhusu matokeo mabaya ambayo waliyoyapata katika michezo mitatu iliyopita.

Katika andiko lako alilolitoa leo, Mwafulango aliwaomba mashabiki na wapenzi wao kuwa watulivu na kuliachia benchi la ufundi lifanye kazi yake wakiamini bado wanaweza kubadilisha matokeo mabaya wanayoyapata katika michuano ya ligi kuu.

''Matokeo tunayoyapata hatuyapendi ila inatulazimu kuyakubali na kuangalia wapi tumeteleza hadi kuyapata' ni kweli inatuuma ila tuamini tutarekebisha, tunawaachia waalimu wafanye kazi yao tutatoka hapa tulipo kwa kishindo'' alisema.

Baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na wadau ni kumwomba Mkurugenzi wa timu hiyo ambaye pia ni meneja wa timu hiyo kujiweka pembeni na kuliacha benchi la ufundi lifanye kazi yake maana kitendo cha yeye kuwepo kwenye benchi la ufundi linampunguzia nguvu ya kuwahoji makocha matokeo yanayojitokeza.

Pia wamemwomba mkurugenzi wa timu hiyo James Marwa Bwire kwenye dirisha dogo kuongeza wachezaji wengine wazoefu ambao watakuja kuongeza nguvu wakishirikiana na wachezaji vijana walipikwa hapo kwenye kituo cha Alliance School Academy.

Sambamba na hilo wameliomba benchi la ufundi kubadilisha mfumo wanaotumia kwa sasa wa kucheza pasi fupifupi na kulazimisha kupita katikati ya uwanja na kuanza kutumia pasi ndefu kwa kupitia pembeni mwa uwanja ili kupata magoli, huku wakiwataka wawape washambuliaji mbinu mbadala za kufunga magoli maana mipira inawafikia ila kutumbukiza kimiani ndio wanashindwa.

Alliance amecheza mechi tatu hadi sasa akipoteza mechi mbili na kutoka sare mechi moja kitendo ambacho kimeibua minong'ono mingi kutoka kwa mashabiki na wakereketwa ambao wanaisapoti timu yenye maskani yao kata ya Mahina wilaya ya Nyamgana Mkoani Mwanza.

SHARE THIS

Facebook Comment

0 comments: