Monday, August 27, 2018

Wanalambalamba wawalambisha koni tatu wababe wa masau bwire
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC,  imeendeleza wimbi la ushindi kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) baada ya usiku wa jana kuipiga Ndanda mabao 3-0.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, ikiwa imefikisha jumla ya alama sita katika mechi mbili ilizocheza hadi sasa.

Azam FC iliingia kwenye mchezo huo ikimkosa nahodha wake,  Agrey Moris,  aliyepata maumivu kidogo ya kifundo cha mguu kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City ambao ikishinda mabao 2-0 na nafasi yake ilichukuliwa na David Mwantika.

Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, ilishuhudiwa Azam FC ikianza kwa kasi kubwa na kufanikiwa kutawala kipindi chote ikicheza soka safi la kasi na pasi fupi fupi na ndefu.
Azam FC ilianza kwa kujipatia bao la uongozi dakika ya 41 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na kiungo mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu, penalti iliyotokana na beki wa Ndanda, Malika Ndeule,  kuunawa mpira wakati akijaribu kuokoa krosi iliyopigwa na Ramadhan Singano 'Messi'.

Kutinyu aliongeza tena bao la pili dakika ya 60 akiwapita mabeki wa Ndanda kabla ya kumtungua kipa akimalizia krosi safi iliyochongwa na Kangwa.

Winga Joseph Mahundi, aliyekuwa kwenye kiwango kizuri alihitimisha ushindi wa Azam FC kwa kufunga bao safi pembeni kwa shuti akimalizia pasi safi ya Nahodha Msaidizi Frank Domayo 'Chumvi', aliyekuwa nahodha wa mchezo wa leo.

Mara baada ya mchezo huo, wachezaji wa Azam FC wanatarajia kupumzika kwa siku mbili kabla ya kuanza rasmi maandalizi ya mchezo unaokuja dhidi ya Mwadui utakaofanyika Uwanja wa Mwadui, Shinyanga Septemba 14 mwaka huu.
Azam FC ilitakiwa kucheza mchezo ujao wa ligi Ijumaa hii dhidi ya Ruvu Shooting, lakini umeahirishwa kupisha maandalizi ya timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' inayotarajia kucheza na Uganda 'The Cranes' kufuzu Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.
Wachezaji wa Azam FC walioitwa Stars ni mshambuliaji Yahya Zayd, Nahodha Agrey Moris na kiungo Mudathir Yahya.
Nyota wengine walioitwa timu zao za Taifa ni beki wa kulia Nickolas Wadada (Uganda) na Tafadzwa Kutinyu (Zimbabwe).
Kikosi cha Azam FC:
Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, David Mwantika, Mudathir Yahya, Joseph Mahundi/Salmin Hoza, Frank Domayo (C), Danny Lyanga, Tafadzwa Kutinyu/Yahya Zayd, Ramadhan Singano/Salum AbubakarSHARE THIS

Author:

Facebook Comment

0 comments: