Friday, August 31, 2018

Mwenge wa uhuru wapokelewa jijini Mwanza kuzindua miradi mbalimbali.


MWANZA
Mwenge wa Uhuru umewasili katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza ukitokea katika Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema kwa ajili ya kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza Dkt. Philis Nyimbi amepokea Mwenge huo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya Sengerema Mwl. Emmanuel Kipole na kubainisha kwamba miradi itakayopiwa na mbio za Mwenge ina thamani ya shilingi bilioni 4.8.

Mapokezi hayo yamefanyika mapema leo Agosti 31, 2018 katika eneo la Kamanga Feri ambapo Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Ndg. Charles Francis Kabeho ametumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi na walezi kutimiza wajibu wao kwa kuwapa mahitaji muhimu ya shule watoto wao katika kipindi hiki ambacho serikali inatekeleza mpango wa elimu bure ili kuwawezesha kupata elimu bora.

Aidha ameonya kuhusu suala la dawa za kulevya kwa vijana ambapo amewataka kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya kwa kuwa yanahatarisha maendeleo ya taifa na kuwahimiza kuwa wazalendo.

Baada ya makabidhiano hayo, Mwenge wa Uhuru umeelekea Kata ya Isamilo na kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara ya Isamilo-Nyashana-Jeshini inayojengwa kwa kiwango cha mawe yenye urefu wa kilomita moja kabla ya kuwasili katika eneo la Soko Kuu katikati ya Jiji la Mwanza ili kukagua shughuli za kiuchumi za vikundi vya vijana na akinana pamoja na kukabidhi hundi ya shilingi milioni 200 kwa vikundi 52 vya wajasiriamali vya akina mama na vijana.
CHANZO----------------BMG

SHARE THIS

Facebook Comment

0 comments: