Sunday, August 26, 2018

Barua ya wazi kwa Kamati ya waamuzi nchini, jitazameni upya.

Mwandishi Wetu @FMG
Mwanza

Wasalaam Wadau wa Michezo popote mlipo katika Nchi ya Tanzania. Tunamini mko salama sana na mnaendelea vyema na ujenzi wa taifa katika nyanja zote kwa nguvu zote bidii na juhudi. 

Kwanza tuchukue fursa hii kuwapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya katika kuendeleza soka nchini, kwa weledi umakini juhudi na bidii katika kuhakikisha kwamba michuano mbalimbali inapata matokeo sio ya kulalamikiwa ila matokeo yanayotokana na ubora wa kikosi, mbinu za makocha na uhodari wa wachezaji.

Kama wadau wa soka nchini tumeguswa tuwaase Kamati ya Waaamuzi pamoja na waamuzi walioteuliwa kuchezesha ligi kuu, ligi daraja la kwanza na ligi daraja la pili kuwa wakweli na kuongeza umakini katika uchezeshaji wao wa michuano mbalimbali hapa Nchini.

Msimu miwili kama zio mitatu iliyopita zilisikika sauti za baadhi ya makocha wa timu wakilia na nyinyi kuwa hamtendi haki katika baadhi ya michezo, mnaamua matokeo pasipo kuaca timu iliyo bora ishinde kitendo kinachovunja nguvu harakati za kupandisha kiwango cha soka letu nchini.

Ligi kuu ya msimu huu ndio imeanza ila kuna baadhi ya viashiria vinavyotia shaka hasa katika baadhi ya mechi zilizochezwa na kuanza kuibua maswali kwa baadhi ya wadau wa soka kuwa kwa hali hii haki itatendeka kweli au basi hakuna haki yoyote.

Kwa jicho la uamuzi tunaamini mmepewa mafunzo na maelekezo ya soka linataka nini, huku mkiongozwa na sheria kumi na saba za soka hivyo hatutegemei kuanza kuona mambo yanayoanza kukanganyana mapema hivi na kuanza kuibua minong'ono mapema hivi kuwa kuna timu zinabebwa na zingine hazibebwi huku suala hili likihushishwa na viashiria vya rushwa.

Mathalani kuna mechi kama ya Singida na Mwadui, Mwamuzi alikataa goli lililofungwa na Mwadui kusawazisha na mechi ya Coastal Union na Biashara, Mwamuzi alikataa goli la Biashara ambalo hatujui kuna utata wa namna gani.

Kamati ya Waamuzi kupitia Mwenyekiti wa Kamati Salum Chama, nyinyi ndio walezi na wapangaji wa waamuzi kwenye michezo mbalimbali inayosimamiwa na TFF kupitia bodi ya ligi, kuweni makini na msikubali baadhi ya waamuzi wachache kuwachafua wakati mnafanya kazi kwa weledi kabisa.

TFF kupitia Mkurugenzi wa Mashindano Ephraim August na Katibu Mkuu Wilfred Kidana Secretarieti yake jitahidini kumulika katika hili mapema na kuwabaini waamuzi wachache wabovu wanaotaka kuvuna wasipopanda, ili waziache timu zilizojiandaa vizuri vipate ushindi na sio kupendelea kusiko na maana.

Msipokuwa makini hapa tutashuhudia lawama kubwa huko mbele na watalaumiwa na kila mdau wa soka kwa kushindwa kuwajibika katika kuweka uwiano mzuri wa suala la uchezeshaji wa mechi mbalimbali.

SHARE THIS

Facebook Comment

0 comments: