Wednesday, July 18, 2018

TAIFA STARS KUCHEZA KOMBE LA DUNIA 2030...Na Mandala J.

Leo nimeona kuwa wote tuliojipa timu za kushangilia kwenye kombe la dunia tumeonesha kuwa tunapenda mpira sana na tulikuwa tayari kuvaa utaifa wa nchi zingine na tuliusaliti Utanzania pasipo na gharama yoyote na hii ilionesha kwa namna mpira wa miguu ulivyo na nguvu katika maisha ya kila siku ya watu wengi, na hata wale ambao hukutaraji kuwa ni mashabiki wazuri wa mpira majumbani walichagua timu au Utaifa wa nchi mbili au moja.

Namkumbuka Admn wangu mmoja katika kundi letu aliandika majina ya wanagroup na kuwaambia wamwambie ni timu gani wanazoshangilia kombe la dunia kila mwanagroup akataja baadae alisema kila mtu aliechagua timu ikitoka mbele ya jina lake kutaandikwa RIP. Ilikuwa ni ubunifu ulioleta radha na adimu wangu huyo ndio bingwa wa kombe la dunia.

Kwa moyo tulioutumia kusaliti taifa letu Leo naomba kugawa majukumu ya ili Taifa starz icheze kombe la dunia na kila alieshabikia nchi yoyote atapaswa kushiriki kuonesha mapenzi yake ya mpira tunataka mwaka 2030 tukacheze kombe la dunia.

Hili ntaligawa kimkoa , mikoa yetu Tanzania iko 31 na wachezaji wanaotakiwa kombe la dunia ni 23 tu hivyo idadi ya mikoa yetu ni mingi kuliko idadi ya wachezaji huo ndio ukweli kabisa.

Mwanza pale panaonekana kulikuwa na washambuliaji wazuri akina Fumo feliciani , Nteze John Lungu, Sanifu Lazaro Tingisha tunawaombeni nyie wanamwanza tutengenezeeni mshambuliaji mmoja tu mzuri kwa gharama zenu na mipango yenu mmoja tu  .

Kigoma pale alikuwepo Said Sued Scud, Edibily Jonas Lunyamila pale Kidahahwe tunaombeni na nyie mkoa mzima mtutengenezee mshambuliaji mmoja tu mkoa mzima mmoja tu.

Mbeya nyie kihistoria mna wachezaji warefu na wameshiba akina Godfrey Katepa, Jimmy Morred tunaombeni nyie Wanyakyusa wote mtutengenezee kiungo mmoja wa maana yaani mkata umeme ikiwezekana kama Ngolo Kante.

Ruvuma na Mtwara nyie unganeni  kwa akina Razack Yusuph Careca, Steven Mapunda , Mohamed Hussein Mmachinga jamani wanantwara tunaombeni winga wa kulia wa maana sana ndio mchango wenu mkubwa.

Tabora huku kwa akina Ally Mayai Tembele, Ahmed Mwinyimkuu tunaombeni kiungo wa kushambulia mmoja tu ndio kazi yenu tunataka 2030 tukacheze kombe la dunia hatutaki masihara aisee.

Dodoma tunawaomba sana tena sana Kwa akina Athumani Chuji nyie hata beki anatutosha mtafuteni anapopatikana sijui ni kondoa , Mpwapwa, Bahi, Kongwa ila tunamtaka sentahafu aliekamilika na msisahau kumwambia mweshimiwa Majaliwa Kasimu Majaliwa , Mzee wa kubana matumizi sijui atakuwa Dar au Dodoma nae anahusika kwani hataki kupiga Daba na mmoja wa wachezaji watakaocheza kombe la dunia. Tukumbuke nia ya kwanza ni kwenda kushiriki na sio kushindana na ikitokea tumefunga goli moja huku tukifungwa magoli hata 1000 tutakuwa tumepata mafanikio makubwa sana kwanza 8bn ya ushiriki tutarudi nayo.

Dar es salaamu hapa ndio watu walipo ila tunawaombeni mabeki wawili , mmoja wa kulia na mwingine wa kushoto maana kwenu ni jukumu dogo sana tunaombeni mabeki kwelikweli na msituangushe na mkoa utakaotuangusha tutajua la kuufanya kikubwa tunataka kucheza fainali kombe la dunia mwaka 2030. Tukumbuke sijui mtawaandaaje ila kikubwa namwamini mkuu wa mkoa kijana mwenzangu Paul Makonda mtafanikiwa kiurahisi sana nia kombe la dunia 2030.

Zanzibar kuna mafundi sana na wanazalisha mafundi sana tunaombeni mchezaji fundi kwelikweli aliekamilika kuliko Hazard kwa Zanzibar yote kuchagua na kututengenezea mchezaji mmoja mnaweza sijui mtamuweka wapi au mtawaweka wapi kama ni Brazil, Ujerumani , Croatia akafunzwe na Ivan Rakitic, Ivan Perisic au Mtakatifu Modric mtajua nyie ila kikubwa jukumu lenu mlitekeleze kwa uweredi mkubwa iwe Mara 10 ya Makame au Mudathiry.

Mkikosa basi awe beki Mara zaidi na zaidi ya Agrey Morris na Canavarro .

Kwani Joseph Katuba, Stephen Names, Mohammed Mwameja walitokea wapi mikoa iliotoa makipa hawa jamani ni jukumu lenu tunaomba kipa anaewazidi hawa ni jukumu pia.

Haiwezekani mikoa iwe 31 tushindwe kupata wachezaji 23 wa kutuwakilisha kombe la dunia nchi ina wakazi laki tatu( Iceland) imecheza kombe la dunia sie 56m tunashindwaje.

Mi nimechoka kuisaliti nchi yangu Mara Leo Mcroatia, Mfaransa, Mbelgiji, Muargentina, Mbrazil, Mara Muruguary , Mara Muingereza kumbe Niko kwenye kochi nimekaa Tukuyu nakula ndizi na parachichi.

Kama tuliweza kuwekeza muda na akili na pesa kulipa vibanda umiza kushangilia wenzetu na kujipa uraia tuombaneni kutekeleza mpango kazi huu wa kimkoa. Unaekataa kushiriki tukutenge ndani ya mkoa wetu maana tunahitaji kucheza kombe la dunia.

Mungu ibariki ndoto hii.

+255659797279
+255620639779

SHARE THIS

Facebook Comment

0 comments: