Tuesday, July 31, 2018

Mvuvi anaswa na Nyavu haramu Wilayani Sengerema.Edson Sadock
Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza  linamshikilia, Robert Charles, miaka 40, mkazi wa chifunfu wilaya ya Sengerema Mkoa wa Mwanza kwa kosa la kupatikana na nyavu haramu (timba) 52 za kuvulia samaki pamoja na samaki wachanga wenye ukubwa wa chini ya sentimita 50 wenye thamani ya tshs. 500,000/= wakiwa kwenye mfuko wa sandarusi, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Awali  polisi walipokea taarifa toka kwa wasamaria wema kwamba katika kijiji tajwa hapo juu wapo  watu  wanajihusisha na shughuli za uvuvi haramu, na askari walifanya ufuatiliaji wa haraka kwa kufanya doria na misako katika maeneo hayo na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa tajwa hapo juu akiwa na nyavu haramu aina ya timba 52  zote zikiwa  chini ya sentimita  5 pamoja na samaki wachanga wenye ukubwa wa chini ya sentimeta 50, wenye thamani ya tshs. 500,000/=

Jeshi la Polisi lipo katika upelelezi na mahojiano na mtuhumiwa, pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani, aidha upelelezi na msako wa kumtafuta  mtuhumiwa mwingine aliyekimbia pamoja na  watu wengine wanaojihusisha kwa namna moja au nyingine katika  shughuli za uvuvi haramu  bado unaendelea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishina wa Polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa wakazi wa jiji na Mkoa wa Mwanza, amewataka kuacha kujihusisha na shughuli za uvuvi haramu kwani  ni kosa la jinai na vilevile anaendelea kuwasisitiza wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu mapema ili waweze kukamatwa na kufikishwa Mahakamani.


SHARE THIS

Facebook Comment

0 comments: