Wednesday, June 20, 2018

WARAKA WANGU KWA WAZIRI DR HARRISON MWAKYEMBE.Na Mandala J.

Heshima kwako kiongozi wangu  kitaifa na kijimbo , nakuandikia waraka huu nikiwa Mbambo nikitokea Kyela kupitia Ipinda na Ntaba.

Kama unavyojua huu ni mwezi wa sita nilienda nyumbani kula mbasa kidogo wale samaki watamu na wazuri kutoka Ziwa Nyasa , pamoja na hayo naomba nikupe hongera sana kwa namna mambo unavyoyaendesha kwasasa katika Wizara ya Michezo na Utamaduni, wakati wa uteuzi wako kwakukuangalia mi binafsi nilitumia taswira yako kuona kama itakuwa kazi ngumu kwako nikasahau kuwa we ni Dr na umedhihirisha hilo mpaka ninapoandika waraka huu.

Waraka huu naomba uusome na ufikirie namna sahihi kisheria jinsi ya kufanya na kupitia mchakato wa kisheria mpaka bungeni na kuupitisha na kuwa sheria , najua ni kazi ngumu lakini kwa namna ya Watanzania walivyochoka kutokupata matokeo katika michezo ya kimataifa wakiwemo wabunge kama Watanzania itawezekana na ni imani yangu hatujachelewa mpaka sasa.

Naomba uangalie namna ya kuunganisha Sera yetu ya uwekezaji nchini na Sera ya mpira wetu kwenda pamoja ili kuleta namna sahihi ya kufaidi rasimali tulizobarikiwa na Mungu kwa Multiplier effects.
Nilipokuwa naenda Kyela nilipoouona mgodi wa makaa ya mawe pale Kiwira ilinifikirisha tena na tena kuwa kuna uwezekano wa kufanya Sera ya mpira wetu na Sera ya uwekezaji kwenda pamoja na kupata matokeo chanya.

Ikiwa kama yeyote anaetaka kuwekeza katika nyanja yeyote atapaswa kuwa na timu ya watoto , iwe ili uweze kuwekeza Tanzania utapaswa kuwa na timu ya mpira ya watoto kati ya miaka 9-18. Kwa maana hii kuwa kama ni Acaccia watapewa mkataba wa uwekezaji sharti la kuwekeza ni pamoja na kuwa na timu ya watoto yenye umri wowote na kuwa na kocha mwenye sifa awe mzalendo au kocha wa kigeni. Sasa tuje tuone kwenye madini nchini kwetu kuna makampuni mangapi ya kigeni yaliowekeza tuchukulie yapo 15 tayari tutakuwa na timu za watoto kumbi na 15 ambazo makamppuni haya yatazihudumia kwa kila kitu na zifanye usajiri wa watoto na kwakuwa elimu ya Tanzania ni bure na watoto wengi watakuwa katika umri wa shule watasoma au utaratibu mzuri wa namna ya watoto kupata elimu uigwe kama Alliance schools wanavyofanya kwa watoto wanaokuwa nao pia.

Tukija kwenye usafirishaji nako pia makampuni ya ndege, majini pia labda kuna makampuni 7 tutakuwa na timu saba za watoto nazo hivyo hivyo,  tuje kwenye hizi shule kubwa kama Tanganyika International school na zinginezo za aina hiyo kama Feza nako kuwe na shule 10 Tanzania tutakuwa na timu kumi pia.

Tuje makampuni ya kupakua mizigo kutoka kwenye ndege pia labda makampuni 3 nako tutakuwa na timu 3, makampuni pale bandari pia hivyohivyo kwa maana ya kwamba unawekeza Tanzania kwa industry yoyote utapaswa kuwa na timu ya watoto ambayo utaihudumia kwa kila kitu na kikubwa ni kuwa na kocha wa kiwango anaeendana na umri husika na kocha atahudumiwa na kampuni husika.

Kwa hesabu ya haraka tutakuwa na timu zisizopungua 100 za watoto Tanzania katika mfumo sahihi wa kujifunza kama kila timu itakuwa na watoto 20 basi tutakuwa na watoto 2000 katika mfumo wa mafunzo sahihi ya mpira.

Kwakuwa makampuni yatagawiwa watoto kulingana na umri basi watatembea katika mikono ya makocha katika makuzi yao ya mpira.

Mabenki  na financial institution bila kuishau BOT kama kielelezo jumla 50 wawe na timu zao bado makampuni ya bia yako 5 bado makampuni ya vyakula hivyo hivyo Coca cola na Pepsi pia ili mradi unawekeza iwe ni FDI ( Foreign Direct Investment) au Indirect , franching, Partnerships au njia yoyote sheria ya kuwa na timu ya watoto iwe ni lazima.

FAIDA ZAKE.

Kupanua wigo wa ajira mbadala kwa vijana wetu katika miaka ijayo na kuwafanya kupata elimu ya mpira wakiwa katika umri sahihi kama kwa wenzetu ilivyo na mfano halisi angalia clip inayotembea mwaka 1998 Antoine Grizmanne akiomba sahihi ya Robert Pires na Barthez Leo ndio mshambuliaji bora pale France baada ya miaka 20.

Tutazalisha akina Mbwana Samatta wengi sana na kuwa na uhakika wa timu yetu ya Taifa kufanya vizuri siku za usoni na huu ni kama mradi ambao tunauwekeza kwa manufaa ya Taifa.

Kuendelea kupata faida ya rasimali zetu kama nguzo ya maendeleo na kuendelea kushare ile faida ya mwisho ya makampuni ya kigeni wanayoondoka nayo ( Patriation profit).

Kuongezeka kwa miundo mbinu bora kwa maana ya kwamba timu zitakuwa nyingi na kuzidi miundo mbinu na kwa usumbufu kuna makampuni yatahitaji kuwa na viwanja vyao na yatatengeneza viwanja na mwisho wa siku tutapata viwanja vingine .

Ajira kwa makocha wazawa na kuifanya taaluma ya ukocha kuwa taaluma muhimu sana na kuipanua kwa kutoa mafunzo Mara kwa Mara.
Tutakuwa tumelipunguzia taifa gharama ya kuandaa wanamichezo wa mpira kwa vitendo na fedha pia na kuacha alama sahihi ya chama tawala juu ya michezo nchini maana mafanikio kwa njia hii ni lazima yatapatikana. Tusisahau wakati Tanzania tunatamba katika michezo mbalimbali timu zilikuwa za mashirika au makampuni na sio wanachama kwa mfumo huu tunarudi kulekule lakini katika mfumo wa kisasa zaidi.

Watoto kupata elimu ya darasani na elimu ya mpira na kikubwa ni kufanya akili za watoto hawa kuwa katika hali nzuri zaidi kutokana kuwa na mazoezi , ukiangalia sana watoto wengi shule hawajishughulishi na michezo na mwisho wa siku kutojua vipaji vyao lakini kwa mfumo huu watoto wengi watajiingiza katika michezo na kujenga taifa bora la sasa na baadae.

UENDESHAJI.

Serikali kama serikali wataunda chombo maalumu cha kusimamia hili na wajiriwa wake kulipwa kwa pesa za TFF na hasa mgawo wa FIFA maana ni njia sahihi ya kuendeleza mpira nchini. Wasipewe TFF kwa maana ya kwamba isije kuwalemea kusimamia kuhakikisha hizi timu zipo na zinafanya kazi kulingana na sheria iliowekwa, na kwa maana ya kwamba kama BOT watakuwa na timu ya watoto pia TFF watapaswa kuwa na timu pia, football association pia za mikoa iwe ni sheria kwao kuwa timu .

Chombo hicho kianzishe mashindano yoyote ili kujenga hali ya ushindani kati ya makampuni husika na kutengeneza upinzani wa kushindana kwa faida ya kujenga hari ya ushindani kwa vijana wetu na kujenga hali ya kupambana kwa ajili ya uzalendo. Kwa namna ilivyo mashindano haya yatapata udhamini mzuri kwa faida ya kwamba makampuni yatajua kuwa ni mashindano yanayokutanisha makampuni mengi na watoto au vijana ni wengi na wazazi wao au ndugu zao watakuwa wanafuatilia hivyo kutoa fursa ya matangazo na biashara pia na kwa hili basi mafanikio ya mashindano ni dhahiri.
Kijiogrofia kutoa kipao mbele kwa maaneo yanayozalisha aina Fulani ya wachezaji tunaowataka kama vile warefu, wenye miili kuendana na hitaji la mpira wa kisasa , kwa ukusanyaji wa wachezaji huu tunaweza kupata wachezaji wahitaji la Taifa katika mashindano mbalimbali.

Kwa shule zilizopo kuwepo na mpangilio wa shule za michezo kwa ngazi ya kijiji, tarafa, wilaya, mkoa na Taifa ili kuweza kupata muunganiko sahihi wa michezo , ili kama kuna mtoto hayumo katika mfumo wa wawekezaji basi atapatikana katika mfumo wa shule ya kuwa kuwepo na shule maalumu kimichezo yaani pale kijijini, tarafa, wilaya, mkoa , kitaifa kwa shule za msingi na sekondari na uzuri walimu wapo na shule zipo ni suala la kuteuwa na kujenga utamaduni wa usimamizi sahihi.

Nisikuchoshe linaweza kuwa wazo la mwanzo litakalozalisha wazo pia.

Joseph Mwamboja Mandala.
SLP 1249
Dodoma.

+255659797279
+255620639779

SHARE THIS

Facebook Comment

0 comments: