Tuesday, June 12, 2018

WANAHABARI ACHENI KUONGEZA CHUMVI KWENYE HABARI MNAZOZIANDIKA.

“KAMANDA WA POLISI MKOA WA MWANZA NAIBU KAMISHINA WA POLISI AHMED MSANGI ANATOA RAI KWA BAADHI YA WAANDISHI WA VYOMBO VYA HABARI HUSUSANI BLOGU NA MAGAZETI AKIWATAKA KUACHA TABIA YA KUONGEZA CHUMVI KATIKA UANDIKAJI WA TAARIFA ZAO AMBAPO KATIKA TUKIO HILI BAADHI YA VYOMBO VYA HABARI VIMEDAI KUWA KUNDI LA POLISI NDIO LILILOMKAMATA MAREHEMU, HUKU VYOMBO VINGINE VIKIDAI KUWA KUNDI LA ASKARI NDILO LILILOMSHAMBULIA MAREHEMU KITU AMBACHO SIO KWELI, HIVYO ANAWAOMBA WAANDISHI KABLA YA KUANDIKA TAARIFA ZAO WAWE WANAULIZA KWANZA ILI KUWEZA KUPATA UKWELI WA TAARIFA TOKA PANDE ZOTE MBILI”
Oscar,
Husika na maneno niliyoyawekea wino mweusi kama msisitizo wa uzito wake hapo juu.
Ni muhimu taarifa zote zinazoenda kwa umma kuwa za kweli na kuandikwa kwa usahihi na kwa wakati muafaka.
Siyo nia yangu kutetea upotishaji. La hasha!
Lakini nacheea kusema 'upotoshaji' kama kweli upo, basi lawama zote zielekezwe kwako binafsi ukiwa mshauri wa RPC kwenye masuala ya habari na Ofisi ya RPC mwenyewe kwa kukalia habari ambazo ni muhimu kufikishwa umma au umma unahitaji kuzifahamu kwa undani na usahihi wake.
Mfano dhahiri ni tukio hili ambalo Ofisi ya RPC inadai kupotoshwa na Media. Tkio limetokea tangu Juni 9, tena wilaya jirani ya Misungwi ambako mtu anaweza kwenda na kurudi mjini ndani ya muda wa saa moja. Lakini Ofisi ya RPC inatoa taarifa hiyo siku mbili baadaye, yaani Juni 11.
Inawezekana na hakika ninajua kuna taratibu za kukamilishwa na Polisi kabla ya kutoa taarifa kwa umma. Lakini haiwezekani taratibu hizo kuchukua muda wa siku mbili kukamilika.
Jeshi la Polisi linahitaji kubadilika na kutenda kwa kasi ya maendeleo ya teknolojia iliyogeuza dunia kuwa kijiji kwa taarifa kusambaa kama moto wa nyika.
Najua unafahamu miongoni mwa vigezo muhimu vya habari ni Timing. This is one of the main factors kwa mwandishi na chombo chochote cha habari kinachojitambua.
Nashauri sote tutimize wajibu kwa kila mmoja ili kuondoa misigano isiyo ya lazima inayodhoofisha afya ya umoja, ushirikiano na weledi. 
Ofisi ya Kamanda isikalie habari hata kama haipendezi machoni mwa jeshi hilo kwa sababu kutoipenda na kuikalia hakutavizuia vyombo vya habari na waandishi makini kufikia habari hizo.
Ni heri Ofisi ya RPC kuzitoa kwa mukhtadha inayoona inafaa kuliko kujaribu kuzipotezea kwa sababu kufanya hivyo kutazaa 'upotoshaji'
Nasi vyombo vya habari na waandishi tutatimiza wajibu wetu kama tufanyavyo mara zote kwa kutafuta ukweli wa habari na tips tunazozipata kutoka kwa watoa habari wetu. Tunapokosa ushirikiano kutoka Ofisi ya RPC huku tukiwa tumejiridhisha na usahihi wa tukio, tutaendelea kutimiza wajibu wetu na hivyo RPC kubakia kutoa ufafanuzi kama ilivyotokea kwa tukio hili la Misungwi. Sidhani kama hii ni afya sana kwetu sote waandishi na Jeshi la Polisi.
Tubadilike kwa kila upande kuthamini, kujali na kuheshimu wajibu, weledi na uwajibikaji wa kila upande.
Polisi toeni taarifa kwa wakati. Nasi vyombo vya habari tukizipata kabla yenu, tutawauliza na tunaomba mtupe ushirikiano hata kama habari hiyo ‘siyo nzuri’ kwenu.
Natoa ushauri huu kwa nia njema na moyo thabiti wa kuona vyombo vya habari na Jeshi la Polisi ambao ni wadau muhimu kwa kila mmoja tunafanya kazi bila kusigana kwa sababu sote tunahudumia umma. Tanzania ni yetu sote. Kila mmoja atimize wajibu kujenga Taifa tunalolitaka. Mungu ibariki Mwanza, Mungu ibariki Tanzania!
Peter Saramba Ongiri,
Mwananchi Communications Ltd.
Ofisi ya Kanda ya Ziwa Victoria.
Mwanza.
12/06/2018.
+255766434354.

SHARE THIS

Facebook Comment

0 comments: