Very Recent Posts

Friday, October 26, 2018

HABARI | WASANII WA BONGO FLAVA KUANZA KUIMBA MUZIKI WA INJILI.

HABARI | WASANII WA BONGO FLAVA KUANZA KUIMBA MUZIKI WA INJILI.

Staa wa Muziki wa Injili kutoka Nchini Tanzania anayetamba na video yake mpya iitwayo Kishindo Irene Robert amefunguka mbele ya blog ya Famara News na kusema kuwa ''anaanzisha kampeni ya kuhamasisha vijana wanaoimba muziki wa Bongo Flava waaanze kuimba muziki wa injili''.

Alisema kuwa amekuwa na mzigo huo kwa muda mrefu wa kutaka waimbaji hao wanaoimba muziki huo wa Bongo Flava wakibadilika ili waanze kumwimbia Mungu na waache kuimba nyimbo alizoiita nyimbo za Mapenzi. ''Vijana wengi wana sauti nzuri sana lakini wanamwimbia mtu asiye na majibu katika mahitaji yao'' alisema Irene Robert.


Irene alisema kuwa kwa sasa ameanza kufanya mawasiliano na baadhi ya wasanii hao ili kuanza kuwapa neno la uzima ili watumie sauti zao kwa njia nzuri ili waanzae kumtukuza Mungu na sio kumtukuza miungu mingine. Irene alisema hapendi kuona wasanii wazuri wenye sauti nzuri wanaendelea kuimba muziki huo ambao hauna manufaa katika na kukupa uzima wa milele.


Irene ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kishindo Investments na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Kishindo Foundation alisema kupitia taasisi zake ana mpango wa kufanya mambo makubwa katika nchi ya Tanzania na nje ya Tanzania maana Mungu amempa neema na kibali na sauti nzuri ili aweze kumtumikia na kuisaida jamii. Pia kwa sasa alisema kuwa ameanza kuzalisha tisheti ya jina lake Kishindo ili kuwafikia watu wengi zaidi. Pamoja na hilo alisema bidhaa nyingi zinakuja kutoka kwake kikubwa wananchi waendelee kumwombea na kumkubali ili afike mbali. 

KUTAZAMA VIDEO YA WIMBO WA IRENE ROBERT KISHINDO HUU HAPA CHINI. Utakumbuka IRENE ROBERT juzi kati alifunguka katika Exclusive Interview mbel ya kamera ya AYO TV na Millard AYO na kuzungumzia kutamani kuwaona wasanii wa muziki wa kizazi kipya (Bongo Flava) kuanza kuimba muziki wa Injili ambao utamtukuza Mungu. TAZAMA INTERVIEW HIYO HAPA CHINI.

Thursday, October 25, 2018

UZINDUZI WA TAARIFA YA TAKWIMU ZA VIASHIRIA VYA MALARIA NCHINI.

UZINDUZI WA TAARIFA YA TAKWIMU ZA VIASHIRIA VYA MALARIA NCHINI.


HOTUBA YA MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KATIKA UZINDUZI WA TAARIFA YA UTAFITI WA VIASHIRIA VYA MALARIA WA MWAKA 2017 NCHINI TANZANIA (2017 TMIS) KATIKA UKUMBI WA KARIMJEE TAREHE 22 OKTOBA, 2018

·          Dkt. Mpoki M. Ulisubsya, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto;
·          Katibu Mkuu Wizara ya Afya - Zanzibar;
·          Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu,
·          Bi. Mayasa Mwinyi, Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
·          Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Marekani,
·          Wawakilishi kutoka Mashirika ya Umoja wa Mataifa;
·          Wakurugenzi wa Wizara na Viongozi Mbalimbali wa Serikali,
·          Maofisa wengine wa Serikali,
·          Wadau kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu,
·          Wadau wetu muhimu Wanahabari,
·          Wageni Waalikwa
·          Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya na kutuwezesha kujumuika pamoja leo. Pili, niwashukuru Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi kwenye shughuli hii muhimu ya Uzinduzi wa Taarifa ya Utafiti wa Viashiria vya Malaria ya mwaka 2017. Sote tunatambua kuwa, Sekta ya Afya ni miongoni mwa sekta muhimu katika jamii yetu katika kuchangia ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini na hususan katika kutekeleza Malengo Endelevu ya Maendeleo ya mwaka 2030 na Agenda ya Afrika ya mwaka 2063.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Matokeo ya utafiti huu yatasaidia Serikali ya Awamu ya Tano na wadau wengine katika kutathmini na kufuatilia utekelezaji wa mipango endelevu katika huduma za afya zinazoendelea kutolewa hapa Nchini. Kwa kifupi utafiti huu una umuhimu wa kipekee katika Wizara yangu kwani matokeo yake yatatusaidia katika kujitathmini hatua zilizofikiwa katika kupambana na ugonjwa wa malaria na kujipanga vizuri ili kufikia azma ya kuitokomeza ifikapo mwaka 2030.  Kama tunavyojua ugonjwa wa Malaria ni  ugonjwa ambao ni hatarishi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii na unasababisha kuyumba kwa utoaji wa huduma za jamii katika nchi yetu. Ugonjwa huu umeendelea kusababisha maradhi na vifo nchini na kwa mujibu wa takwimu ya sasa inaonesha kuwa, katika kila wagonjwa 100,000 wa malaria 9 kati yao hufariki  na makundi ya jamii yaliyo katika athari Kubwa ya malaria ni watoto na wajawazito. Ni Dhahiri kuwa mtoto anapoumwa na malaria inawalazimu wazazi au walezi kusimamisha kazi zote za kiuchumi ili kumuuguza na kushughulikia matibabu. Hivyo, ni Dhahiri kuwa Ugonjwa huu unachangia katika kuzorota kwa ukuaji uchumi katika Sekta zote na Maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Serikali kwa kupitia programu za kudhibiti malaria kwa Tanzania Bara na Programu ya Kumaliza Malaria ya Zanzibar wamefanya juhudi kubwa ya kupunguza malaria nchini. Serikali pia imetunga sera na mikakati mbalimbali ili kuweza kumaliza kabisa Malaria ifikapo 2030.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Katika mada fupi iliyotolewa na wataalam imeonesha matumaini na mwelekeo mkubwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano katika suala zima la kudhibiti malaria nchini. Viashiria vingi vimeonesha matumaini makubwa katika Sekta ya Afya na hii imetutia nguvu ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii na maarifa zaidi kwa lengo la kuboresha huduma zinazotolewa kwa Wananchi kupitia Sekta ya Afya. Pamoja na matumaini hayo makubwa, bado kuna maeneo ambayo yanahitaji kuendelea kuboreshwa zaidi kwa kushirikiana na wadau wote ili tuitoe Nchi hapa ilipo na kuipeleka katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Nina imani na mtakubaliana nami kuwa suala la maradhi haliwezi kuachiwa Serikali peke yake, bali ni la sisi sote kwa umoja wetu. Hivyo, changamoto zilizoanishwa katika taarifa hii zitahitaji juhudi za ziada na pengine kujitathmini kwa kina ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Nitumie fursa hii kuelezea jitihada za Wizara yangu kupitia Serikali ya awamu ya 5, inayoongozwa na Mhe. Dkt John Pombe Magufuli katika kutekeleza mikakati mbalimbali ya kupambana na ugonjwa wa malaria kama ifuatavyo;

Uchunguzi na Matibabu ya ugonjwa wa Malaria;
Tumeongeza kasi ya upimaji ili kuhakikisha kuwa wagonjwa wanaodhaniwa (suspected) kuwa na malaria, wanapimwa kwa kutumia kipimo kinachotoa majibu kwa haraka (mRDT) au hadubini; kutumia dawa mseto (ACTs) pale mgonjwa anapothibitika kuwa na vimelea vya malaria kwa kuzingatia maelekezo ya mtoa huduma.

Kinga Dhidi ya Malaria
Wizara imeendelea kuhakikisha kuwa kila mwananchi anajikinga na malaria kwa kutumia vyandarua ambavyo vimekuwa vikisambazwa bila malipo kwa wananchi kupitia Kampeni mbalimbali nchini. Kwa sasa Wizara inaendelea kutekeleza Mpango endelevu wa ugawaji vya ndarua (Continuous distribution) kupitia wanafunzi wa shule za msingi na kupitia Kliniki za wajawazito na watoto, ambayo hujulikana kama Chandarua Kliniki ambapo hadi sasa jumla ya vyandarua milioni 31vimeshagawiwa nchini kote.

Katika kutekeleza Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, kuhusu Afua ya kuangamiza viluwiluwi vya mbu katika mazalia, Wizara imeshirikiana na OR-TAMISEMI kuratibu zoezi la usambazaji wa viuadudu katika Halmashauri za mikoa 14 yenye mambukizi makubwa ya malaria jumla ya lita 236,750. Aidha, kupitia OR-TAMISEMI, Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, inaendelea na utekelezaji wa Afua hii.

Tiba – Kinga kwa Wajawazito (SP);
Katika kuhakikisha kuwa wajawazito wanakingwa dhidi ya madhara yatokanayo na malaria, Wizara imeendelea kuwapatia wajawazito vyandarua na dawa-kinga ya Sulphadoxine Pyrimethamine (SP) kwa vipindi maalumu wanapokuwa wanahudhuria Kliniki.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Wizara  kwa kushirikiana na wadau ina utaratibu endelevu wa kufanya tathmini ili kuweza kupima ufanisi wa Sera na Mikakati ya malaria tuliyojiwekea ili kujua mafanikio ya utekelezaji wa mikakati hiyo katika jamii. Wizara  pamoja na Wizara ya Afya -Zanzibar kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo ilifanya Utafiti wa Viashiria vya Malaria (Tanzania Malaria Indicator Survey 2017), ili kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa programu za udhibiti wa Malaria nchini.
Madhumuni ya utafiti huu, yanalenga kutoa taarifa za kiwango cha maambukizi ya malaria katika jamii, kutathmini umiliki, upatikanaji na matumizi ya vyandarua; upatikanaji wa huduma ya kinga dhidi ya malaria kwa wajawazito; utambuzi wa dalili za awali za malaria kabla ya kupata huduma ya matibabu; kujua njia na dawa zinazotumika kutibu malaria kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano; kupima ufahamu na uelewa kuhusu ugonjwa wa malaria, jinsi ya kuzuia na tiba sahihi.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Siku ya leo kupitia hafla hii, nitazindua rasmi matokeo ya kina ya Utafiti wa Viashiria vya Malaria kwa Mwaka 2017. Napenda nizungumzie mafanikio ambayo yameelezwa katika mada iliyopita. Mojawapo ya matokeo ya utafiti huu ni pamoja na umiliki na upatikanaji wa vyandarua vyenye dawa katika ngazi ya kaya. Matokeo yameonesha kuwa asilimia 78 ya kaya nchini Tanzania zinamiliki angalau chandarua kimoja chenye dawa. Katika utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2015-16, ni asilimia 66 tu za kaya zilikuwa zinamiliki angalau chandarua kimoja chenye dawa. Umiliki wa vyandarua vyenye dawa ni wa kiwango cha juu kwa kaya za mijini (asilimia 81) ikilinganishwa na kaya za vijijini (asilimia 77).

Kwa upande wa Tanzania Bara, Mkoa wa Pwani ndio unaoongoza kuwa na kiwango kikubwa cha umiliki wa vyandarua vyenye dawa (asilimia 89). Mkoa wa Njombe una kiwango kidogo cha umiliki wa vyandarua vyenye dawa (asilimia 58) ikilinganishwa na mikoa mingine. Kwa upande wa Zanzibar, Mkoa wa Kusini Pemba una kiwango kikubwa cha umiliki wa vyandarua vyenye dawa (asilimia 90) na Mkoa wenye kiwango kidogo cha umiliki ni Mjini Magharibi (asilimia 73). Aidha, sote tunatambua kuwa watoto na wanawake wajawazito wapo katika hatari kubwa ya kuugua malaria, hivyo, ni muhimu kutumia vyandarua ili kuzuia malaria. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa, asilimia 55 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 na asilimia 51 ya wanawake wajawazito walilala kwenye chandarua chenye dawa usiku wa kuamkia siku ya utafiti. Vile vile, katika kuzuia malaria, wajawazito wanatakiwa kupata dawa ya malaria aina ya SP/Fansidar kama kinga dhidi ya malaria.
Pia, matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa, ni asilimia 26 tu ya wanawake wajawazito wenye umri wa miaka 15-49 waliojifungua watoto hai miaka miwili kabla ya utafiti walitumia dozi tatu au zaidi za SP/Fansidar (IPTp3+) wakati wa ujauzito wao. Kiwango cha wajawazito waliotumia dozi tatu au zaidi za SP/Fansidar wakati wa ujauzito wao ni kikubwa katika maeneo ya mijini (asilimia 31) ukilinganisha na maeneo ya vijijini (asilimia 24).

Ndugu Wageni Waalikwa,
Napenda kuwakumbusha kuwa, tarehe 25/04/2018 ilikuwa ni Siku ya Malaria Duniani na Kitaifa siku hii iliazimishwa Wilayani Kasulu, mkoani Kigoma. Katika siku hiyo nilipata pia wasaa wa kuzindua matokeo muhimu ya utafiti huu, ambapo tuliona kuwa kiwango cha malaria kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano nchini Tanzania kimeshuka kwa Zaidi ya nusu kutoka asilimia 14.4 mwaka 2015 hadi asilimia 7.3 mwaka 2017. Hii ni kwa kutumia kipimo cha haraka cha utambuzi wa vimelea (mRDT).

Miongoni mwa mikoa ya Tanzania Bara, utafiti huu unaonesha Mikoa yenye kiwango kikubwa cha watoto wenye malaria ni, Kigoma (asilimia 24.4), Geita 17.3%, Kagera 15.4%, na Mtwara 14.8% ambapo Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Njombe, Songwe, Dodoma na Mikoa yote mitano (5) ya Zanzibar ina kiwango kidogo cha maambukizi chini ya asilimia moja. Vile vile, Halmashauri zifuatazo zina maambukizi ya kiwango cha juu Kakonko 30.8%, Kasulu DC 27.6%, Kibondo DC 25.8%, Uvinza 25.4%, Kigoma DC 25.1%, Buhigwe 24%, Geita DC 22.4%, Nanyamba TC 19.5%, Muleba DC 19.4%, Mtwara DC 19.1%,  na Halmashauri zenye  maambukizi ya kiwango cha chini ya asilimia 0.1 ni Mbulu TC, Mbulu DC, Hanang, Hai, Siha, Moshi MC, Mwanga, Kondoa TC, Meru DC, Arusha CC, Arusha DC,  Munduli, Ngorongoro, Rombo DC,  
Ndugu Wageni Waalikwa,
Kama nilivyosema wakati wa maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani takwimu hizi, zinaonesha kupungua kwa kiwango cha malaria kwa kiasi kikubwa, na hii ni habari njema kwetu sote na inaonesha ni jinsi gani Serikali yenu ipo tayari kutoa kipaumbele katika kuhakikisha kuwa malaria inadhibitiwa na hatimae tuweze kuitokomeza kabisa. Ili kuhakikisha lengo hilo linafanikiwa, tunapaswa kufanya kazi kwa pamoja katika kufikia malengo tuliyojiwekea ili jamii, hasa watoto chini ya umri wa miaka mitano na wajawazito ambao ndio waathirika wakubwa wa ugonjwa wa malaria waweze kuepukana na ugonjwa huu.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Zaidi ya kupima malaria, watoto pia walipimwa kiwango cha damu. Matokeo yanaonesha kuwa asilimia 3.6 ya watoto wa umri wa miezi 6-59 wana upungufu wa damu. Kwa upande wa Tanzania Bara, Mkoa wa Kagera unaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha watoto wenye upungufu wa damu asilimia 6.9, na Mkoa wa Iringa una kiwango kidogo cha watoto wenye upungufu wa damu, yaani chini ya asilimia moja. Kwa upande wa Zanzibar, asilimia 6.5 ya watoto katika Mkoa wa Kaskazini Pemba wana upungufu wa damu, na Kusini Unguja, ni chini ya asilimia moja.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Napenda kuchukua fursa hii kuwafahamisha kuwa matokeo haya niliyoyasema ni sehemu ndogo tu ya takwimu zilizokusanywa katika utafiti huu wa Viashiria vya Malaria wa mwaka 2017. Taarifa za kina zinapatikana katika ripoti kubwa ambayo nitaizundua hivi punde ili iwe tayari kwa ajili ya matumizi ya kupanga na kufuatilia mipango mbalimbali tuliyojiwekea.Ndugu Wageni Waalikwa,
Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kupunguza kiwango cha malaria kwa zaidi ya nusu, bado tuna changamoto, ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi ili kwa pamoja tuweze kufikia malengo ya kutokomeza malaria nchini. Wanajamii kutotumia vyandarua ipasavyo katika kujikinga na ugonjwa wa malaria, kuwepo kwa mitazamo potofu juu afua za kupambana na malaria; mfano dhana ya kuwa viuatilifu-ukoko vya kunyunyizia ukutani zinaleta kunguni na viroboto na kuwa vyandarua vinapunguza nguvu za kiume. Hizi zote ni dhana potofu ambazo hazina ukweli wowote. Vilevile, Jamii kutoshiriki kikamilifu katika kutunza mazingira na kuharibu mazalia ya mbu kwa kufukia madimbwi, kusafisha mifereji, kuweka mazingira katika hali ya usafi na kuharibu mazalia ya mbu kwa kuondoa maji yaliyotuama.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Natambua kuwa nyie kama wadau katika utafiti huu, mna majukumu na pia maeneo tofauti mnayoyashughilikia. Hivyo, matokeo ya utafiti huu ni muhimu sana katika kuhakikisha kuwa takwimu zinatumika kwa kiasi cha kutosha na wadau wote katika kutekeleza sera na mipango mingine ya kimaendeleo. Hivyo basi, matokeo haya yachukuliwe kama changamoto katika juhudi za kumaliza tatizo la malaria nchini.  Hivyo, tunapaswa kufanya kazi kwa pamoja katika kufikia malengo tuliyojiwekea ili kuweza kuokoa maisha ya watu wetu na hasa watoto chini ya miaka mitano, wanawake wajawazito na nguvu kazi ya Tanzania kwa ujumla.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Kabla sijahitimisha hotuba yangu napenda kutambua michango mbalimbali iliyowezesha kukamilika kwa utafiti huu. Nianze kwa kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa kufanya Utafiti huu.  Pili, nawashukuru timu ya wataalam kutoka Wizara zote zilizoshiriki, waratibu, wasimamizi, wadadisi na Wananchi kwa ujumla kwa kuwezesha kufanyika kwa kazi hii muhimu na nzuri. Tatu, napenda kutambua juhudi zilizofanyika chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Afya - Zanzibar, Wataalam kutoka Shirika la ICF la Marekani, na kwa namna ya kipekee napenda niwashukuru Global Fund na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kwa kutoa msaada wa fedha zilizotumika kutekeleza utafiti huu. Pia niwashukuru wadau wengine wa afya kwa kutoa wataalam na ufuatiliaji mzima wa utafiti huu.

Niwashukuru pia Wananchi kwa kukubali kushirikiana vyema na wataalam wa afya, na hapa nitumie fursa hii, kuwaomba kuendelea kushirikiana na Serikali yenu katika kukabiliana na changamoto zilizoibuliwa katika utafiti huu. Wote kwa pamoja na kwa niaba ya Wizara yangu napenda kuwashukuru sana.

Ndugu Wageni Waalikwa,  
Pia napenda niwakumbushe wakati tunaadhimisha siku ya Malaria Duniani kule Kasulu – Kigoma niliiagiza Ofisi ya Taifa ya Takwimu iandae kiwango cha Malaria kwa kila Halmashauri na kuendelea na juhudi za kuzisambaza kwa wadau wote hususan Waheshimiwa Wabunge ili iwasaidie kuweka mipango mikakati ya kupambana na ugonjwa wa malaria katika maeneo yao.

Hitimisho
Napenda kuchukua nafasi hii kwa namna ya kipekee kabisa kuipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar na Watalaam wengine kutoka Wizarani kwangu kwa kukamilisha kazi hii muhimu. Niseme tu kuwa nimefurahi sana kusikia taarifa hii ipo tayari na leo hii pia nitaizindua ili iweze kuanza kutumika, ninawapongeza sana kwa kazi nzuri.

Baada ya maelezo yangu napenda sasa kutamka rasmi kuwa: NIKO TAYARI KUZINDUA TAARIFA YA MATOKEO YA UTAFITI WA VIASHIRIA VYA MALARIA WA MWAKA 2017 NCHINI TANZANIA.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.